Our

Articles

Ndi Umunyarwanda: Msingi wa Falisafa ya Umoja kwa Wanyarwanda

Go Back

21 October 2021

Zaidi ya Miaka 27 imepita sasa tangu yafanyike Mauaji ya Halaiki ya Kimbari yaliyolenga jamii ya Watutsi nchini Rwanda.

Ni mauaji yaliyogharimu uhai wa Wanyarwanda zaidi ya Milioni Moja wasio na hatia na kuiacha jamii ya Wanyarwanda katika hali tete bila matumaini kabisa ya mustakabali wa taifa lao.

Mwaka huu (2021) imetimia miaka 25 tangu jumuiya ya Unity Club - Intwararumuri ianzishwe.

Hii ni jumuiya inayowakutanisha kwa pamoja Mawaziri waliopo madarakani na Mawaziri wastaafu pamoja na wenzi wao (wake/waume). Kwa Pamoja viongozi hawa huunganisha fikira na mawazo yao ya busara kukabiliana na changamoto zinazolikabili taifa ili waweze kutoa  suruhisho la kudumu na lenye manufaa kwa taifa.

Unity Club ilianzishwa mwaka 1996, na Mheshimiwa Jeannette Kagame, mke wa Mheshimiwa Paul Kagame, Raisi wa sasa wa Jamhuri ya Rwanda. Akiwa na lengo la kujenga umoja wa Wanyarwanda kupitia viongozi wa juu ambao wamekuwa msitari wa mbele kutoa nuru na mwangaza (touch bearers) katika kuhamasisha jamii nzima (wazee na vijana) kuwa na umoja na uzalendo wa kweli, ili kulijenga taifa moja lenye nguvu, upendo na mshikamano.

Kupitia Jumuiya hii ya Unity Club, viongozi waliopo madarakani na wastaafu kutoka matabaka mbalimbali ya Wanyarwanda, kwa pamoja wamekuwa mfano bora katika kusimamia na kuenzi  maadili mema kwa jamii ambalo ndilo lengo kuu la Unity Club, pamoja na kuchangia  katika kujenga Umoja na Maridhiano miongoni mwa Wanyarwanda ili washirikiane katika kujenga jamii imara kwa maendeleo ya taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Jeannette alijua wazi kuwa Umoja ni Nguvu na Utengano ni Udhaifu na taifa la Rwanda lilikuwa na udhaifu mkubwa tangu awali katika suala hilo la kuwaunganisha wananchi jambo ambalo kulirekebisha ilihitajika ubunifu wa hali ya juu na mkakati wa kipekee katika mchakato mzima wa Serikali kuliunganisha taifa la Rwanda.

Kupitia mipango mbalimbali iliyoanzishwa na jumuiya hii ya Unity Club, wajumbe walitumia njia mbalimbali kujenga na kurudisha utu na upatanishi miongoni mwa jamii ya Wanyarwanda ikiwa ni pamoja na kupewa nasaha na mawaidha juu ya umuhimu wa umoja na mshikamano wa kitaifa ili kurekebisha makosa yaliyotokana na uwepo wa Sera za Kibaguzi zilizochangia kuwatenganisha Wanyarwanda katika matabaka yaliyochochea uhasama miongoni mwao.

Mheshimiwa Jeanneatte Kagame aliona ni vyema agenda hii ikaanzia kwa viongozi wa juu kama Mawaziri na familia zao ili kujenga umoja na uaminifu kati yao ili iwe rahisi kufikisha ujumbe huo kwa jamii kwa ujumla.

Ndi Umunyarwanda (Mimi Ni Mnyarwanda) ni programu (Mpango) mmojawapo kati ya mingi iliyobuniwa na kupewa kipaumbele chini ya jumuiya ya Unity Club ili kurejesha umoja na uaminifu katika jamii ya Wanyarwanda baada ya Mauaji ya Halaiki ya Kimbari ya mwaka 1994.

Katika Makala hii mpango huu wa Ndi Umunyarwanda utagusiwa na kujadiliwa kwa kina ili kuweka bayana maana na misingi yake.

Tafsiri rahisi ya neno Ndi umunyarwanda ni Mimi ni Mnyarwanda. Kwa mtazamo wa harakaharaka unaweza kujiuliza endapo Wanyarwanda kweli wanahitaji kukumbushwa uraia wao. Lakini kwa kuiangalia historia ya nchi ya Rwanda, tangu enzi za ukoloni na hata baada ya taifa kupata uhuru wa bendera, sera za kiutawala zilighubikwa zaidi na  ubaguzi na viongozi walijikita zaidi katika kuwafundisha wananchi tofauti zao badala ya umoja wao. Hii ilikuwa kabla ya ukombozi wa Rwanda uliofanywa na wanajeshi wa RPA wa kulitoa taifa mikononi mwa uongozi dhalimu mnamo mwaka 1994.

Awali watu walitambuliwa kwa Ukabila zaidi (Mhutu, Mtutsi na Mtwa) na mbaya zaidi watu walipewa fursa ya elimu ama ajira  kwa misingi ya ukabila na ubaguzi wa kikanda ambao ulishika hatamu.

Ilifikia mahali hata kitambulisho cha taifa (National Identity Card) kilikuwa na taarifa za kibaguzi za kikabila, na kikanda kama ilivyoainishwa hapo juu.

Ni dhahiri kabisa kwamba ubaguzi ulikuwa umekithiri kwa kiwango cha kutisha, ambapo harakati za viongozi kuitenganisha jamii zilipelekea kwa kiasi kikubwa kutokuaminiana, watu kutopata haki zao za msingi kwa sababu tu ya upande huu na sio ule.

Lilikuwa ni jambo la kawaida na viongozi waliona fahari kuwapendelea tu wale waliowataka wao pengine kwa kuwa wanatoka nao sehemu moja au kabila lao ni moja. Hii ilipalilia uhasama na chuki miongoni mwa Wanyarwanda  

Baada ya ukombozi wa taifa uliofanywa na Jeshi la RPA likiongozwa na Jemedari Mkuu  Paul Kagame, kurejesha utaifa badala ya ukabila, ilikuwa ni kazi kubwa na ilihitaji mipango na mikakati  isiyo ya kawaida kuanza kuijenga Rwanda yenye  umoja, upendo na mshikamano.

Zilihitajika mbinu madhubuti kukabiliana na majeraha ya aina mbalimbali iwe ya kimwili ama ya kisaikolojia. Ikumbukwe kwamba baadhi waliopoteza familia, ndugu jamaa na marafiki katika mauaji ya halaiki ya Kimbari dhidi ya Watutsi na wengine wakiuguzia majeraha makubwa yaliyopelekea ulemavu wa kimwili na hata kiakili,wajane na yatima wengi.

Wapo waliohusika katika mauaji ya Kimbari, au ndugu zao walihusika na walikuwa wanakabiliwa na mashitaka na adhabu kutokana na udhalimu huo. Wengine walikuwa wamezagaa huku na kule wakitafuta hifadhi ya ukimbizi. Wote walikuwa ni raia wa nchi ambayo haina hata taasisi moja inayofanya kazi na miundombinu yote ilikuwa imeharibiwa vibaya.

Kwa hiyo, kupitia Ndi Umunyarwanda  ilikuwa ni fursa mpya inayowakumbusha na kuhamasisha Wanyarwanda kuwa na umoja na kujiona kama taifa moja lenye mwelekeo na lengo moja la kujenga nchi yao upya.

Uhamasishaji ulifanywa kupitia makongamano, warsha na vikao mbalimbali , na vyombo vya habari kama magazeti, majarida, radio na runinga.

Vijana, watoto na watu wazima wote walihusishwa ili kila mwananchi aweze kuwa na haki sawa na uwajibikaji katika kujenga taifa lake.

Kama ilivyoelezwa hapo awali, Unity Club - Intwararumuri kwa ushikiano na Tume ya Taifa  ya Umoja na Maridhiani (National Unity and Reconciliation Commission) walianzisha Ndi Umunyarwanda programu mwaka 2013.  Wajumbe wa UC walikuwa mstari wa mbele katika shughuli zote za uhamasishaji ndani na nje ya nchi hasa kupitia kwa Mabalozi kusudi hata Wanyarwanda walioko nje wasipitwe na fursa hii ya kuelewa ukweli na kuwa pamoja na wenzao katika kutafuta suluhu ya matatizo yanayoikabili nchi yao kama mchango wao wa kulijenga upya taifa la Rwanda.

Mafanikiyo ya Ndi Umunyarwanda.

Ilikuwa ni safari ndefu lakini yenye matumaini makubwa. Katika hiyo safari ambayo ni dhahiri kuwa bado inaendeleza mpango wa Ndi Umunyarwanda ambapo Programu ilifanikisha mambo mengi hasa kujenga na kukuza umoja wa Wanyarwanda na kurudisha hali ya kuaminiana na muhimu zaidi, kutoa mwongozo wa maadili mema kwa vijana ambao ni taifa la leo na kesho na ni nguzo muhimu kwa ustawi wa taifa lolote.

Katika utafiti uliofanywa  mwaka 2020 kuangalia mchango wa Ndi Umunyarwanda katika kuleta umoja na maridhiano,  matokeo yanatia moyo, asilimia 98 ya waliohusika wanakubaliana kwamba kuna mchango mukubwa wa Ndi Umunyarwanda katika kujenga na kuimarisha umoja na uaminifu miongoni mwa Wanyarwanda. Na asilimia 98 wanakubali kuwa  Ndi Umunyarwanda imechangia kwa kiasi kikubwa kuwa na maadili mema miongoni mwa jamii. 

Hivi sasa dhana ya ukabila na sera za ubaguzi zimepigwa marufuku.  Kitambulisho cha taifa na  cha kusafiria (passport) havina chembechembe za kibaguzi za kabila wala dini ya mmiliki wa vitambulisho hivyo.

Kupitia mpango huu wa Ndi Umunyarwanda, kumekuwa na michakato mbalimbali ya kuwakutanisha kwa mazungumzo ili kuombana radhi na kuridhiana kufuatia mauaji ya Kimbari  yaliyowalenga Watutsi. Mchakato huo umepelekea watu hao kuishi pamoja kwa upendo na kusaidiana.

Wale ambao vidonda vyao bado ni vibichi au wanaugulia majeraha ya kihistoria kutokana na maovu ya sera chonganishi zilizowazilizowatenganisha Wanyarwanda  wanaendelea kuuguza vidonda au makovu na wana matumaini ya kupona na kuwa na taifa moja lenye umoja na mshikamano katika kizazi hiki na vizazi vijavyo.

Wahenga walisema “Usione vyaelea vimeundwa”, Rwanda na Wanyarwanda baada ya janga la mauaji ya Kimbari dhidi ya Watutsi mnamo mwaka 1994, ilikuwa ni jamii iliyosamabaratika. Miaka 27 baadae, leo Wanyarwanda wana matumaini ya maisha na wanauona mustakabali wao na wa taifa lao.

Hii inatokana na ukweli kuwa hivi sasa kupitia sera thabiti na mipango maridhawa kama huu wa Ndi Umunyarwanda na mipango mingine iliyopewa vipaumbele na serikali na wadau mbalimbali ikiwemo jumuiya ya Unity Club, wananchi sasa wanaishi kwa Amani na kuaminiana lakini yote haya hayajatokea kwa miujiza, bali ni mazao ya juhudi chanya na mikakati ya kipekee ya kuitoa nchi kwenye lindi la umasikini na  sera za kikabila na ubaguzi wa kikanda, ikawa nchi ambayo kila Mnyarwanda ana haki sawa na uwajibikaji katika kujenga Rwanda mpya.  

Unity club - Intwararumuri chini ya uongozi wa Mheshimiwa Jeannette Kagame ikishirikiana na taasisi nyingine za kitaifa imechangia kwa kiasi kikubwa katika kujenga umoja na maridhiano miongoni mwa Wanyarwanda.

Mimi ni Mnyarwanda!

Waandishi:

Coletha Uwineza RUHAMYA –  Mjumbe wa Unity Club &

Hon. Oda GASINZIGWA – mjumbe wa Unity club na mbunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

More Updates

News and Events

Read News and Events by the Unity Club

Go to News and Events

Publications

Read and Download Publications by the Unity Club.

Go to publications
© 2024 Unity-Club
Developed by Awesomity Lab